Thursday, October 25, 2007

Yanga....This is too much


Yanga Looooooooooooh Too much wazeeeee


SHILINGI milioni 50 walizopewa na mfadhili wao, Yusuf Manji hazikufaa kitu mbele ya wachezaji pungufu wa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Bao la Ulimboka Mwakingwe(MWENYE UZI MWEKUNDU NYUMA YAKE NI LULANGA MAPUNDA) alilofunga dakika ya 30 lilitosha kuipa Simba ushindi wa bao 1-0 na kuifanya ifikishe pointi 14.

Simba ikiwa na wachezaji kumi baada ya beki wa kati, Henry Joseph kupewa kadi nyekundu dakika ya 15, ilipata bao hilo baada ya Ulimboka Mwakingwe kupewa pasi na Nurdin Bakari na kabla ya kufunga winga huyo mfupi alivuta hatua mbili akapiga shuti kali ambalo lilipita kwenye kwapa za Ivo Mapunda na kugonga mwamba kabla ya kujaa nyavuni.
Mchezo huo ulifanyika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na kuhudhuriwa na mashabiki wengi wakiwamo wengi kutoka jijini Dar es Salaam.

Manji ambaye yupo nchini Marekani aliwapa Yanga Shilingi milioni 40 kwa ajili ya maandalizi ya mechi hiyo huku akiwapa wazee Sh milioni kumi za kufanyia 'shughuli' za maandalizi.
Mchezo huo ulichezeshwa na Othman Kazi wa Dar es Salaam aliyesaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha na Ismail Mshana wa Dodoma.

Ulikuwa ni mchezo wa tatu kwa Kazi kuchezesha mechi ya Simba na Yanga tangu awe mwamuzi na Yanga haijawahi kushinda akiwa yeye mwamuzi.

Mechi nyingine ambazo Kazi alizochezesha kati ya Yanga na Simba ni Simba iliyoifunga Yanga 2-0 katika fainali ya Tusker Julai 2, 2005 jijini Mwanza na nyingine ni ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo iliishia kwa suluhu jijini Dar es Salaam Machi 26 mwaka jana.

Simba walimrudisha katikati Said Sued na kumpeleka Kelvin Yondani katika nafasi ya beki wa pembeni, huku Nico Nyagawa pia akirudishwa katikati kusaidia baada ya kutolewa kwa Henry Joseph ingawa kipindi cha pili Sued alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Soud Abdalla.
Simba ilianza kwa kushambuliwa na ndani ya dakika ya saba, walikuwa tayari wameruhusu kona mbili ambazo hazikuzaa matunda.

Hata hivyo katika mchezo huo, Simba wanapaswa kumpa shukrani kipa wao, Juma Kaseja ambaye alifanya kazi ya ziada kulilinda lango lake.

Shadrack Nsajigwa alipiga kona dakika ya saba, lakini Thomas Morris alipotaka kufunga alijichanganya na kuutoa nje mpira.
Hata hivyo Simba ilijikuta matatani baada ya beki wake wa kati, Henry Joseph kupewa kadi nyekundu na mwamuzi Othman Kazi kwa kumchezea vibaya Thomas Maurice.

Dakika mbili kabla ya mapumziko, Laurent Kabanda angefunga bao, lakini mwamuzi alilikataa mpira uliokuwa umeingia wavuni kwa sababu kipa wa Simba, Juma Kaseja alikuwa amepigwa mtama na wachezaji wa Yanga.
Mechi hiyo ambayo ilihudhuriwa pia na kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo ilishuhudiwa Simba ikienda mapumziko ikiongoza kwa bao moja.

Kipindi cha pili, Simba ilijaza wachezaji wengi nyuma kujihami jambo ambalo lilifanya 'kuzidiwa' mara kwa mara na Yanga ambayo nayo iliamua kupeleka wachezaji wengi kushambulia.
Hata hivyo kujipanga vizuri kwa wachezaji wa Simba kuliwafanya Yanga washindwe kuingia ndani ya eneo la vijana wa Msimbazi ambao waliongezewa nguvu na Julius Mrope aliyekuwa akisumbua sana.
Kabanda wa Yanga aligongana na Kaseja katika moja ya hekaheka na kufanya apelekwe hospitalini.

Yanga ikicheza bila Ben Mwalala na Athuman Idd waliofungiwa na TFF, wameshindwa kulipa kisasi cha kufungwa na Simba kwa takribani miaka mitano.
Mpambano huo ulikuwa ni wa 24 tangu mwaka 2000 huku Simba ikiwa na rekodi nzuri ya kushinda mechi 13 pamoja na ya jana na Yanga imeshinda mara nne tu.
Dakika ya 53, Yanga walitaka kulazimisha bao la kusawazisha baada ya washambuliaji wake kumpora mpira Kaseja na kufunga, lakini mwamuzi alikataa.

Yanga: Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Lulanga Mapunda, Yusufu Hamisi, Wisdom Ndhovu, Credo Mwaipopo, Amri Kiemba/Mrisho Ngassa, Waziri Mahadhi, Laurent Kabanda, Thomas Maurice/Abuu Ramadhani, Amir Maftah/Aime Lukunku.
Simba; Juma Kaseja, Said Sued/Soud Abdalla, Nurdin Bakari, Kelvin Yondan, Henry Joseph, George Owino, Nico Nyagawa, Shaaban Kisiga/Mohammed Banka, Mohammed Kijuso/Julius Mrope, Joseph Kaniki na Ulimboka Mwakingwe.

No comments: