Friday, October 19, 2007

Dah! mwanangu Lucky Dube kadedi kabisaaa!

Wamempiga Risasi jamaa
JOHANNESBURG, Afrika Kusini
WAPENZI wa muziki wa Afrika Kusini jana walikuwa katika siku ya majonzi kutokana na kifo cha kushtua cha mwanamuziki wa reggae, Lucky Dube, 43, aliyepigwa risasi na majambazi waliotaka kumpora gari usiku wa kuamkia jana maeneo ya Rosettenville, Johannesburg.
Msemaji wa Polisi wa Afrika Kusini, Cheryl Engelbrecht alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 8:20 usiku wa kumkia jana wakati mwanamuziki huyo nyota alipokuwa akiwashusha watoto wake wawili katika nyumba ya ndugu yao.
Mwanamuziki huyo alikuwa akiendesha gari lake la kijivu la Chrysler akiwa amewapikia watoto wawili.
Msemaji huyo wa polisi alisema Lucky Dube alikuwa tayari amewashusha mtoto wake wa kiume mwenye miaka 15 na binti yake mwenye umri wa miaka 16 wakati alipovamiwa na majambazi waliokimbia baada ya tukio hiklo wakiwaacha watoto hao bila kuwajeruhi.
"Mtoto wa kiume alikuwa tayari ameshuka kwenye gari. Alipoona tukio hilo alikimbia kuomba msaada" alisema Engelbrecht.
Lucky Dube akiwa amejeruhiwa alijaribu kuondoka gari kwa kasi ili asipigwe risasi nyingine, lakini alipoondoa gari hilo aligonga mti na kufa hapo hapo.
Polisi wa Johannesburg wanawatafuta
watu watatu wanaoendesha gari la bluu Vokiwageni Polo (VW Polo) ambao wanadaiwa kuwa ndio waliomuua msanii wa huyo.
Miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika tukio ni wanamuziki wenzake, Mzwakhe Mbuli, Ringo Madlingozi na Deborah Fraser.
Mbuli alisema: "Ni jambo la kushangaza, wakati nchi inajiandaa kwa fainali za Kombe la Dunia za rubgy, tunapatwa na tukio hili la kusikitisha. Tutashangilia vipi katika hali ya majonzi namna hii, nadhani polisi wanachimba na kuwakatama majambazi hawa."
Mashuhuda walisema kuwa watekaji hao walifungua mlango wa gari na kumpiga Lucky Dube risasi mbili.
"Lucky Dube alijaribu kuondoa gari na akagonga mti na kufariki," alisema shuhuda mmoja na tayari studio ya kurekodia iliyokuwa inamilikiwa na Lucky Dube, Gallo Records imetuma salamu za rambirambi.
"Alikuwa mpole, alikuwa anazungumza taratibu na rafiki mkubwa," alisema Ivor Haarburger, ambaye ni Mkurugenzi wa Gallo Records.
Haarburger alisema Lucky Dube alikuwa mwanamuziki bora reggae bora duniani na aliyekuwa na mashabiki wengi kimataifa nje ya Afrika Kusini.
"Alikuwa mkubwa hata nje ya Afrika, alikuwa anavuta watu 40,000 mpaka 50,000 katika shoo mmoja," alisema Haarburger.
Alisema Lucky Dube amekuwa akizunguka nchi mbalimbali duniani kutangaza albamu yake mpya ijayo ambayo ndio ilikuwa ipo njiani kurekodiwa katika studio hiyo.
Lucky Dube, alizaliwa mwaka 1964, na kupewa jina la "Lucky" kutokana na kuzaliwa akiwa na afya mbovu na madaktari walidhani angekufa siku chache baada ya kuzaliwa.
Lakini Lucky Dube aliishi na kuwa kijana aliyekuwa mstari wa mbele katika muziki wa reggae uliotetea haki za weusi dhidi ya ubaguzi wa makaburu wa Afrika Kusini.
Mwanamuziki huyo ambaye alikuja Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 2000 ametoa jumla ya albamu 20 na alikuwa anajiandaa kurekodi albamu ya 21.
Baadhi ya albamu zake ni Rastas Never Die, Think About The Children, Soul Taker, Trinity na albamu yake ya mwisho ni aliyotoa mwaka jana iliyoitwa 'Respect'.
Mwanamuziki huyo aliyetamba na vibao kama Remember Me, Slave na Prisoners alikuwa havuti sigara,bangi wala kunywa pombe ya aina yoyote.
Licha ya mambo yote ameshinda tuzo mbalimbali 20 ndani na nje ya Afrika Kusini.
Historia yake kwa ufupi ni kwamba Lucky Philip Dube alizaliwa Ermelo, mashariki ya Johannesburg, Agosti 3, 1964.Baada ya mama yake Sara kutaka kuitoa mimba hiyo bila mafanikio, ndipo alipozaliwa Lucky Dube akiwa na afya mbaya. Alizaliwa katika malezi ya mzazi mmoja tu mama aliyekuwa maskini asiyejiweza hali iliyomfanya aishi maisha ya tabu.Wazai wa Lucky Dube walitengana kabla hajazaliwa hivyo kumfanya mama yake kwenda kutafuta kazi sehemu nyingine na kuwaacha Lucky Dube na wadogo zake; Thandi na Patrick wakilelewa na bibi yao.

No comments: