Wednesday, March 26, 2008

Sitaki kabisa hii aibu wala msiniambie!


UKITAKA kuinjoi Bongo basi siku kama hizi za minuso ya sikukuu ndio freshi za kuibuka.
Ndio maana Mzee wa Kutibua hukumbwa na malaria za ghafla pamoja na kuhara kusikoisha ilimradi tu kupata visingizio tosha mpaka wiki ijayo asiibuke kazini.
Nani asiyejua utamu wa tumbo la kuhara bwana...? kumbe mzee mzima niko zangu kwa 'wenyenchi' nkivunja mbavu na kushuhudia viroja.
Ndio nyakati murua ambazo kumfuma mheshimiwa mzima amekwidwa shati na waifu mida ya asubuhi baada ya kuwa bwaksi wala siyo ishu saana Uswazi.
Si alilala kaunta halafu homu ya vitumbua hajaacha?
Kumbe Jumamosi kama hii ya Shopingi ya Pasaka pia ndio wajanja ambao baadhi wamekwenda mbali zaidi kwa kuchongesha suti zao mithili ya maafisa wa benki hujazana Kariakoo na Mnazi Mmoja utafikiri mashushu wa mafisadi.
Wala hakuna cha mashushu ndio staili mpya ya wakwapuaji wa Dasilamu, Bongo kuna mambo!
Kaa naye vibaya halafu akikutoka viwalo vyako spidi atakayochomoka nayo ndio utajua kweli mjini shule.
Ndio mambo ya tawni, we unafikiri ni wote walioulamba unaopishana nao huko katikati ya Jiji wakimwagika jasho wametoka kula vyuku Stiazi?
Watu wako kwenye mishemishe ukizubaa kidogo wakikuingia anga zako ndio umeumia.
Lakini ebu tuache kwanza hizo, hivi kweli hawa jamaa zetu wa hiyo kamati mnayoita ya mashindano wanataka kutupeleka wapi? Mchezaji anamsukuma mwenzake wanamfungia mechi sita za ligi? Wati izi disi!
Unashangaa.. kwani hujaskia yaliyomkumba Emmanuel Gabriel wa Simba wiki iliyopita? Gabriel(pichani) alifungiwa baada ya kutenda kitendo hicho kama mechi dhidi ya JKT Ruvu mjini Arusha.
Lakini kanuni gani hizi zinazotuongoza, mbona huko Ulaya kwenye wenzetu walioendelea tumekuwa tukishuhudia hayo mambo kila siku.
Mara ngapi tumemshuhudia Emmanuel Adebayor wa Arsenal, Jermen Pernant wa Liverpool, Wayne Rooney wa Manchester au hata Joe Cole wa Chelsea wakifanya makosa kama hayo lakini huwezi kusikia kafungiwa mechi sita zaidi ya kuitwa na kuonywa? Hizo adhabu ni kwa manufaa ya nani? au ndio kukomoana tu ili mradi?
Ambacho nilitegemea labda mwamuzi wa ule mchezo Arusha angewaita wote wawili pale pale uwanja na kuwaonya na kama ingezidi sana mmoja wao angepewa kadi ya njano. duh! hii kiboko.
Hilo lilinikera sana nikaamua niliseme kwanza. Lakini kubwa ninalotaka kusema Jumamosi hii ni kwamba hatutaki aibu washikaji, kila kitu mnacho.
Timu ya soka ya Taifa Stars imepangwa kuanza na Kenya Machi 30 kwenye michuano ya kuwania kufuzu Afrika inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani,tunaanzia Nairobi wala hiyo siyo sababu. Kocha wa Stars Marcio Maximo ameshatangaza kikosi chake chenye wachezaji wengi wenye uzoefu mkubwa na ambacho kesho Jumapili kinatinga kambini.
Nimekuwa na imani na kikosi kilichotangazwa pamoja na benchi la ufundi lakini tatizo langu bado lipo kwa wachezaji wenyewe binafsi.
Wachezaji wengi wamekuwa wakichaguliwa wanapoingia Stars wanashindwa kufurukuta huku baadhi wakidai uzoefu na kubaniwa na kocha vinawasumbua. Wengine wanaotoka timu za mikoani wameenda mbali zaidi na kusingizia hali ya hewa.
Ukikaa na kupiga stori na wachezaji walioitwa kwenye vikosi vilivyopita ndio mambo mambo waliyokuwa wakieleza lakini ukiingiza kwenye akili za kawaida hata bila kushtukia(mambo yetu yalee...) jibu la haraka linakuja ni uvivu na kutojielewa.
Wadau wamemwaga manoti kuhakikisha Stars inasonga mbele katika mashindano ya sasa baada ya mwaka jana kushindwa kufuzu kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika yaliyofanyika Ghana.
Wachezaji wanaishi kwenye hoteli ya kifahari kama kawaida, wana basi la kisasa la mamilioni ya shilingi tena lenye kiyoyozi, vifaa vya kutosha, posho tena za kiwango cha juu na kila kitu anachostahili mchezaji.
Sina wasiwasi wala sitaki kuchunguza uwezo wa makocha Wabrazili waliopo lakini wachezaji wanapaswa kufungua akili na kujua kwamba huu ndio wasaa pekee wa kuonyesha makali yao.
Soka ni ajira yao si sehemu ya kufanyia starehe au kujipatia umaarufu. Kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuheshimu nafasi aliyopewa na Maximo na kufanya kazi kikamilifu kwa kutoridhika wala kuvimba vichwa kipuuzi na kupandisha mabega.
Mna kila kitu na sababu tosha za kutufanya tucheke safari hii tumechoka kununa na kuangalia kina Drogba, Ronaldo, Fabregas kwenye video.
Acheni uzembe fungueni akili na muelewe maelekezo mnayopewa ndio kitu pekee kinachoweza kuwafanya mwende huko kwenye mikwanja mikubwa wanayovuta wenzenu 'wa ukweli'.
Kenya haina kikosi cha wachezaji wa ndani watakaotusumbua hivyo, mna uwezo wa kutoa sare kwao au hata kushinda ambayo ndio matokeo tunayohitaji ili kazi iwe rahisi tuwamalizie Nashno Stadiumu tumlie taimingi anayekuja.
Acheni uvivu, tulizeni akili uwanjani muuonyeshe umma kwamba Tanzania inaweza na ina vichwa vinavyolitandaza soka la ukweli ambavyo havistahili kuishia uswahili.
Hakuna cha ajabu. Hii ndio nafasi pekee ya kuchanua Afrika na wachezaji kujijenga na kujiuza nje ya nchi. Tuna kila sababu ya kucheza fainali za Ivory Coast mwaka huu tupambane na waswahili wenzetu jamani tunawaweza kabisa.
Oyaa.. washkaji eee kazeni buti. Wanangu wa Moro kesho siunajua mwanetu Afande Sele anachanga changa karata Dume hapo Mambo Club? Full kujiachia..Tuibuke basi kimtindo Mzee mzima nitakuwemo na wanangu kibao...Siunajua mambo yetu yalee..
0713-374649
momburi2002@yahoo.co

Afande sele noma..! we acha tu.


Afande Sele aikamata tena Morogoro
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
KAMA ilivyotabiriwa awali, Afande Sele kwa mara nyingine juzi usiku alifunika kwenye uzinduzi wa albamu yake ya 'Karata Dume' uliofanyika kwenye ukumbi wa Mambo Club mjini hapa.
Msanii huyo ambaye ni kipenzi cha mashabiki wengi wa hapa, amekuwa na rekodi ya kufanya vizuri kwenye zinduzi zake tatu zilizopita kama ilivyokuwa juzi mbele ya mamia ya mashabiki waliofurika kwenye ukumbi huo.
Si Afande tu wasanii waalikwa kama Jua Cali wa Kenya alifunika na wimbo wake wa 'Kwaheri' huku AY, Dully Sykes, Jaymo na Bwana Misosi nao walikonga nyoyo za mashabiki.
Wasanii Ditto na MC Koba waliorejea kundini hivikaribuni baada ya kupatanishwa na Afande, waliwapagawisha mashabiki walipoimba nyimbo zao za zamani wakati wakiwa kwenye kundi la Gheto Boys.
Afande ambaye alipanda jukwaani majira ya saa nane usiku, alipagawa na makelele ya mashabiki wakati alipoanza kuimba wimbo wake unaovuma wa 'Karata Dume', akavua Jinsi na fulana yake na kubaki na bukta na vesti.

Friday, February 22, 2008

Huu wa Arsenal Wenga ni ukoloni


EBWANA wanangu inakuwaje? Ishu zinaendaje mitaa ya kati hapo, shukrani sana kwa kukodolea macho mitaa hii linakomwaga sera Zee la Kutibua.
Mwanenu lasti wiki ishu zilikuwa nuksi kichizi, mijicho ilikuwa haitaki kuona mambo fulani.
Jamaa zangu fulani ambao hawajaaga Mpwapwa kama Mzee wa Sumo wanaweza kufungasha virago wakidhani ni pua ya mtaalam inafanya mambo yake.
Unafanya mchezo nini? Yaani Red aiyizi noma nakwambia, hata wakaanga sumu macho yao yana nafuu.
Lakini shwari kimtindo Mzee mzima sasa niko freshi napeta zangu kwenye viunga vya Kandoro ambavyo porojo za kifisadi zimepotea kijiweni na kilichobaki ni simulizi mpaka za buti za Bush.
Si baaada ya Bush kutua na midege yake? Palikuwa hapatoshi wana! Hata wauza mihogo wa mtaani kwetu Vingunguti Kiembe Mbuzi walipiga zao mguu na kuibuka Eapoti kumshangaa mshkaji.
Waliobaki uswahili na wenyewe ni vimbwanga tupu, muda wote mijicho haibanduki angani wakishuhudia mihemko na mbwembwe za midege ‘Eafosi wani’.
Wapo wadeni waliobonyeza Mzee wa Kutibua na kumtonya kwamba ujio wa mshkaji umewasevu pia na kuwapa mwanya wa kupishana milangoni kwani wenye mapango walinogewa na soga na kuhamishia bongo zao skani.
Lakini tukiacha porojo hili la FA kutaka kutulelea ligi yao bongo silikubali. Haiwezekani huku ni kutumaliza kabisa pamoja na kidogo tulichonacho.
Wiki chache zilizopita kamati ya Ligi Kuu ya England ilitoa pendekezo na kuonyesha nia ya kutaka Ligi Kuu ya nchi hiyo baadhi ya mechi zake zichezwe kwenye nchi nyingine Duniani ifikapo msimu wa 2010-11.
Rais wa FIFA, Sepp Blatter ameibuka na kupinga mapendekezo hayo kwa kile alichoeleza kwamba ni kinyume na sheria na kwamba itakuwa ni kuangamiza ligi za nchi nyingine.
Jamaa akaendelea kueleza kwamba itatibua pia kampeni za Weldi kapu 2018. Lakini baada yake Aseno Wenga ambaye ni kocha wa Aseno akaibukia kusikojulikana madai yake ni kwamba Blata kachemka.
Anachosema Wenga ni kwamba ligi iruhusiwe kuchezwa nje ili kutangaza zaidi ligi yenye ushindani, kutoa nafasi kwa mashabiki kufaidi uhondo ikiwemo pia kwa klabu husika kujiingiza mamilioni. Mzee Wenga pamoja na Uprofesa wako na hao jamaa wa FA hatutaki.
Lakini wana hii ishu mi sikubaliani nayo! Tukiwaruhusu wakicheza tu Afrika tumekwisha na ndio mwanzo wa kuuwa kabisa ligi na klabu zetu. FA inataka mechi moja ya mwisho kila msimu kwa kila timu ihamishiwe Afrika, Asia au Amerika.
Kwa hali ilivyo sasa mashabiki asilimia kubwa wanabeza ligi zao za nyumbani na kushabikia klabu za England ambazo wanaziona kwenye kideo. Je zikija kucheza hizo mechi zao moja moja Afrika au kwenye hizo nchini nyingine si ndio watatuuwa kabisa na msisimko wote wa mashabiki utahamia Ulaya na kupuuza ligi zao na wachezaji wao?
Hakuna siri kwamba ligi hata klabu nyingi za Afrika bado ni changa na zinahitaji sapoti kubwa ili kuzipandisha katika kiwango ambacho angalau kitakaribiana na wenzetu walioendelea lakini kwa kuwakaribisha wenzetu watumie ardhi yetu ni kupotea maboya.
Tunapaswa kulinda klabu zetu na ligi zetu sasa, Waingereza wametutawala mno kwa kila kitu haiwezekani watuletee mpaka na ligi yao kana kwamba sisi hatuna thamani. Mbona wao hawasemi zetu zikachezwe kwao?
Najua kwa mashabiki ‘walevi’ wa kina Ronaldo wa Machesta, Fabregas wa Aseno au Lampard wa Chelsii hata Gerad wa Livapulu watafurahia wazo la ligi hiyo kuchezwa nje na kuongezwa hadi 39 badala 38 ili wawaone wachezaji wao lakini hasara zake ni nyingi kuliko faida.
Nani atahangaika na Masumbuko wa Mtibwa,Ulimboka wa Simba,Tegete wa Yanga au Mangunguru wa Moro?
Kama lengo lao ni kuja kucheza na klabu zetu kuzipa uzoefu na kubadilishana baadhi ya mambo sawa, lakini si mje mkacheze wenyewe kwa wenyewe.Hakuna faida kwa hilo kwa nchi kama Tanzania zaidi ya kuuwa kabisa ligi yetu. Waingereza wametuletea teknolojia nyingi za kisasa, wametulazimisha kuiga mfumo wao wa maisha tukaachana hata mambo yetu ya kiutamaduni kwa madai kuwa tunakwenda na wakati sasa wamekaa wamefikiria na ligi zetu za ndani hazina maana wameona watuletea zao? Kwanini tukandamizwe kiivyo, lazima tujifunze kuwa maskini jeuri?
Tusikubali kushikwa masikio kwa kila kitu anachoamua mzungu hata kama ni cha kipuuzi, kwa nini ligi yao wasicheze huko huko kwao?
Muda wa kutawaliwa kifikra umekwisha, walishatukalia miaka ya nyuma na kutuweka mifuko mwao, tukajitahidi tukapata uhuru wetu tusiwakaribishe tena watutawale watatuharibia timu zetu za Taifa.
Si wacheze kwenye viwanja vyao sisi tutawaangalia kwenye kideo kwani lazima waje Afrika? Labda Asia na mabara mengine.
Ni changamoto sasa kuwekeza na kuhakikisha ligi zetu zinapiga hatua kwenda kwenye kulipwa waliko wenzetu na tujitahidi kujifunza zaidi kila kunapokucha na tusikubali kuendeshwa na wakubwa kana kwamba sisi hatuna akili wala ujuzi wa kupanga mambo yetu, huu ni ukoloni wa waziwazi.
Mzee wa Kutibua anatia zake nanga mitaa hii, lakini wana..tuibukeni Taifa tukawapige tafu dada zetu wa Twiga Stars, wanatisha kinoma si umeskia leo wanakipiga na mademu wa Kameruni? Tuibuke halafu badaye kama kawa Mugongo...Mugongo..!
Wengine Samaki ana vipande vingapi..!
0713374649
HYPERLINK mailto:momburi2002@yahoo.com
Mzeewakutibua.blogspot.com

Thursday, February 21, 2008

Kikosi cha Mizinga chaanza kutisha


Kundi la Kikosi cha Mizinga cha Jijini Dar es Salaam limeanza kampeni ya kupambana na madawa ya kulevya kwa wasanii wa muziki huo kupitia maonyesho maalum yatakayofanyika kwenye ufukwe wa Coco Beach jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu Kalapina ambaye ni kiongozi wa kundi hilo shoo ya kwanza itafanyika keshokutwa jumapili na wasanii kibao akiwemo Rado watawapiga tafu.

Kikwete- Twiga Stars mnaweza komaeni

RAIS Jakaya Kikwete amewataka wachezaji wa timu yasoka ya wanawake Twiga Stars kucheza kwa kujiaminiwatakapopambana na Cameroon Jumamosi, akisema "mnavyoonekana mnaweza"
Rais Kikwete amesema hayo jana Ikulu jijini Dar Es Salaam wakati wa chakula cha usiku alichowaandalia wachezaji wa Twiga Stars kwa ajili ya kufahamiana kwa kuwa hakupata fursa ya kuwatembelea kambini.
Twiga Stars itapambana na Cameroon katika michuano yaawali ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kuwatoa Eritrea kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2.Fainali za michuano hiyo zinatarajiwa kufanyika Guinea Juni mwaka huu.
Rais alisema: “Mnacheza na Cameroon yenye jina kubwa katika soka la wanaume si wanawake. Hakutakuwepo na Eto’o.
Mtoke hapa muingie kiwanjani mkiamini niko nanyi. Jiaminini na mjue kuwa nyinyi ndio mtakaoshinda na Watanzania wote wako nyuma yenu. Soka la wanawake halina muda mrefu kinachotakiwa ni kujiamini na kuungwa mkono.”

Hii ya Simba ni hatari kubwa


Timu ya Simba imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar na kufikisha pointi 24 ambazo ni hatari kwake kwani katika mechi iliyopita ilitoa suluhu na Manyema United inayokaribia kushuka daraja.

Endapo Simba isipojirekebisha huenda ikampaka faida mtani wake Yanga mwenye pointi 33 ambaye akishinda mechi sita tu kuanzia sasa anamvua ubingwa kwa kufikisha pointi 51 kwani Simba ikishinda zote nane ilizonazo kwa sasa itafikisha pointi 48 tu na kuinua mikono juu. Machupa, Ulimboka mpo?

Aisee.. sijapata kuona hii


Rais Jakaya Kikwete,Makamu wa Rais, Mohamed Shein na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakishangaa jambo wakati walipokuwa kwenye uwanja wa ndege juzi wakimuaga Rais Bush aliyekuwa na ziara ya siku nne hapa nchini.

Sunday, February 17, 2008

Shevchenko arudi AC Milan


AC Milan wanataka kumrejesha Italia mshambuliaji wa Chelsea Andry Shevchenko kwa madai kuwa amekuwa akiwasiliana nao mara kwa mara na wanaamini bado nafasi yake ipo kwenye kikosi hicho.

Simba Full kujiachia, Yanga heee...!


Simba jana ilianza mambo kwenye Ligi ya mabingwa baada ya kuipiga Awassa ya Ethiopia mabao 3-0 kwenye uwanja wa Taifa. Moses Odhiambo kapiga mbili na Ulimboka Mwakigwe moja.

Yanga iliyokuwa Madagascar ikikipiga na As Adema, ilifungwa 1-0 huku ikicheza kwenye mvua kubwa.

Makocha wa Yanga wampa Umbea Milovan


MAKOCHA wa Yanga, Kondic Dusan na Spaso Solokovisk (kwenye picha) wamemweka kitako na kumueleza kila kitu kocha mpya wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic.

Milovan alitua nchini wiki iliyopita alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Wekundu hao kwa mujibu wa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali. Katika mechi ya Ligi Kuu ya Bara, baina ya Prisons na Manyema juzi kwenye uwanja wa Taifa, Kondic, Spaso na kocha wa vijana wa Yanga, Zivojnov Srdan walimchukua kocha Milovan na kukaa nae zaidi ya dakika 25. Prisons ilishinda 4-1.

Hali hiyo ambayo iliwashangaza baadhi ya viongozi wa klabu hizo ambao ilibidi waduwae kwa vile si jambo la kawaida katika miaka ya hivikaribuni kwa makocha wa timu hizo hasimu kukaa na kubadilishana mawazo kwa muda mrefu.Tukio hilo ambalo lilitokea kwenye jukwaa la wageni wa heshima (VIP) wakati wa mapumziko ya mchezo huo lilitokana na makocha hao wenye hadhi ya Uprofesa kufahamiana kiundani kwa miaka mingi tangu wakiwa kwao Serbia.

Miembeni,Chipukizi mdebwedo kabisa


KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini na klabu ya Simba, Trott Moloto ametua nchini akiwa na kikosi cha Mamelodi Sundowns ambayo imeifunga Miembeni ya Zanzibar(pichani) 1-0 katika mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa kwenye uwanja wa Amaan jana jumamosi.

Kwenye kombe la Shirikisho Bufallo ya Zambia imeifunga Chipukizi ya Pemba mabao 5-0. This is too much aiseee 5-0? Ndio kwisha kazi tena.

Huendi mahali sisi ndio Ashanti Utd


"Sisi ndio watoto wa Jiji bwana, mwaka jana simlisema hivyo hivyo tutashuka sisi hatushuki daraja tunazidi kupeta tu mwendo ule ule na wachezaji tutauza kama kawa,"alisema Msafiri Mgoyi ambaye ni rais wa Ashanti United alipozungumza na waandishi wa Blog hii.

Ashanti ina pointi 18 tu na ni miongoni mwa timu nne zinazopewa nafasi kubwa ya kushuka daraja. Nyingine ni Polisi Dodoma, Manyema na Pan Africa ya Kariakoo.


Julio azikunja na Mashabiki Taifa


Kitendo cha mashabiki wa Simba, kumtukana kocha wao msaidizi Jamhuri Kihwelu 'Julio' kilimkera bosi huyo na kuamua kuzikunja baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya mechi wiki iliyopita ambayo matokeo yake yalikuwa suluhu.

Julio(anayetoa lekcha hapo) aliwachenjia mashabiki huku akissisitiza " Najiuzulu nakuachieni timu yenu, hamuwezi kuniletea mambo ya kipuuzi nitakuachieni huyo mzungu wenu...haiwezekani najiuzulu nasema"

Ujasiri wa kufumba macho


LICHA ya kukosa mechi za kimataifa za kujipima nguvu, Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa ya wanawake 'Twiga Stars' Charles Boniface amesema kikosi chake kina mabadiliko makubwa kiuchezaji.
"Naona sasa kuna mabadiliko kiuchezaji lakini kikubwa ni kuanza kujiamini, wachezaji sasa wanajiamini kutokana na kuondoa woga ni mambo madogo tu ya kitoto bado tunajaribu kuyaondoa," alisema Mkwasa.

Lakini licha ya matizi ya kufa mtu yanayopigwa na hawa vijana kwenye uwanja wa Karume bado wataalam wa mambo wanadai ni ngumu kuifunga Cameroon kwa kucheza na timu za Uswazi na wazee wanaotokea Bar kwenye mazoezini.

Hichi kijamaa ni noma-Neville


LONDON, England

BEKI na nahodha wa Manchester United, Gary Neville amewatahadhalisha wapinzani wao wa Kombe la FA timu ya Arsenal kuwa waaangalifu na Cristiano Ronaldo(pichani) kwa sababu anacheza soka ya sayari nyingine msimu huu.
Nahodha huyo Neville ambaye amekuwa benchi kwa muda mrefu msimu kutokana na kuwa majeruhi, amesisitiza Ronaldo sasa ni sawa na nyota wengine wa Red Devils, kama Eric Cantona, Roy Keane na David Beckham.
Neville, 32, alisema: “Katika suala kuburudisha, kutegeneza na kufunga, utapenda kumuona mchezaji huyu akiwa na mpira. Ni mchezaji wa kutoka sayari nyingine.”

Ronaldo kwisha kazi yake


PARIS, Ufaransa

MSHAMBULIAJI Ronaldo de Lima ameendelea kuandamwa na jinamizi la kuwa majeruhi akiwa na AC Milan baadaye kumia mguu na kufanyiwa operesheni itayomweka nje ya uwanja kwa miezi tisa.

Ronaldo alifanyiwa upasuaji huo katika hospitali ya Pieté-Salpetriere mjini Paris ilo fanyika kwa usalama juzi usiku kwa mujibu magezeti ya Ufaransa. Operesheni hiyo ilifanyika saa 3:00 usiku chini ya Professor, Gerrard Saillant ambaye alimfanyia Ronaldo upasuaji wa goti lake la mguu wa kushoto. Baada ya upasuaji huo daktari huyo alielezea jinsi hali ilivyokuwa ya mafanikio.

Fabregas haondoki tena milele


LONDON, Englan

KIUNGO Cesc Fabregas ameingia mkataba mnono wa pauni milioni 33 (Sh bilioni 75) utakaomfanya kuwa moja ya mchezaji anayelipwa zaidi katika historia ya klabu ya Arsenal. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amemtaka kiungo huyo wa Hispania ajitie kitanzi cha kuichezea klabu hiyo hadi 2016 kwa kuongeza miaka miwili katika mkataba wake wa sasa. Fabregas ambaye alikuwa akilipwa pauni 50,000 kwa wiki sasa atalipwa pauni 80,000 kwa wiki. (Pauni 80,000 ni sawa na Sh milioni 180)

Kanye West afunika Grammy

MWANAMUZIKI wa Uingereza, Amy Winehouse na mzoefu Kanye West ndio waliofunika tamasha kubwa duniani la kutuza wanamuziki la Grammy ambalo lilifanyika Jumapili iliyopita ikiwa ni mara ya 50 tangu kuanzishwa.Lakini wanamuziki hao wawili waliikosa tuzo kubwa ya Albamu Bora ya Mwaka iliyonyakuliwa na Herbie Hancock inayoitwa "River: The Joni Letters", ambayo ni mkusanyiko wa nyimbo za mkali wa nyimbo za jazz, Joni Mitchell (ikiwa na wasanii waalikwa ambao ni wapiga gitaa maarufu kama Norah Jones, Tina Turner, na Corrine Bailey Rae).Winehouse, ambaye alitumbuiza kibao chake cha ''I'm No Good'' na ''Rehab'' kupitia luninga akiwa jijini London, nusura atwae tuzo zote alizotajwa kuwania.

Saturday, February 16, 2008

Anelka aibeza Arsenal


Nicolas Anelka amesema: Sisi hatuogopi maneno ya watu, bado Chelsea ina nafasi ya kusonga mbele na kutwaa ubingwa wa England na makombe mengine yote tunayowania."

"Hatuna wasiwasi na upinzani uliopo, sisi jukumu letu ni kushinda na kuwafurahisha mashabiki,"alisema Anelka jana.

Anelka alijiunga na Chelsea hivikaribuni akitokea Bolton.

Arsenal this is too much wazee..!


Licha ya kuwa kinara kwenye Ligi Kuu ya England, Arsenal jana ilichakazwa bao 4-0 na Manchester United kwenye mechi ya kombe la FA. Darren Fletcher kapiga mbili, Nani na Rooney wakamaliza kazi.

Milovan ampa shavu Julio


KOCHA mpya wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic amekiri kuwa ana kazi kubwa ya kuibadili timu hiyo kutokana na kiwango alichokishuhudia katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Manyema, lakini akasisitiza: "Hakuna mabadiliko ya ajabu yanayoweza kuonekana kesho, lakini tutajitahidi".
Simba ilitoka suluhu na Manyema katika mechi ya kwanza ambayo kocha huyo alikaa benchi akisaidiwa ma mzalendo,Jamhuri Kihwelo 'Julio' Jumatano.
Milovan alisema katika mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika leo Jumapili dhidi ya Awassa City ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hatafanya mabadiliko ya kutisha na badala yake kazi kubwa ataifanya Julio.

Simba, Yanga zipo kazini


ZIKIWA chini ya maprofesa kutoka Serbia, Simba na Yanga zinaanza rasmi kazi nyeti za kimataifa zitakapokuwa katika viwanja tofauti kesho Jumapili.
Yanga chini ya Profesa, Kondic Dusan na msaidizi wake Spaso Solokovisk ipo mjini Antananarivo, Madagascar kuivaa AS Adema ya huko kwenye mechi ya raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho.

Simba ya Mtaalam Milovan Cirkovic ipo kwenye uwanja wa Taifa ikiivaa Awassa ya Ethiopia.

Atanyongwa mtu nakwambieni...

MASELA wengine nuksi tu, aheri hata wangebadilishwa na Magunia ya mkaa tukajua moja tu.Bora tu kwani ni nini bwana? Tena laifu ingesonga tu kiulaini kinoma.
Tunawekeana viwingu viwingu vya kizushi bwana laifu lenyewe lipi bwana kibongo bongo na mwendo wetu wa Daladala.
Longolongo nyingi halafu wanatutibulia ishu zetu tu, utafikiri virusi bwana! Kila ukitulia kwenye engo yako unakula zako ‘Uwele’ na wajisiriamali mkipanga mishemishe za hapa na pale wamo, wameibuka na vijimambo vyao, inakuwaje kiivyo wana? Au kuweka maskani ya muda Shamba imekuwa nongwa?
Mara oooh..Mzee mzima hongera bwana nimeona jana waifu katuletea kitu kipya mtaani bwana...
Bado jamaa zinaendelea tu, nkafikiri labda shida ni kilauri nikawachapa moja moja ili wasepe na ishu zao. Bwana si wakazidi kumwaga umbea bwana...? Mara oooh... nimeskia jamaa unamuoa tena nanihii bwana inakuwaje mbona hivyo...!
Si wakazidi kuniganda bwana...mpaka wakaniachia Redi Aizi rafiki yangu. Naiti naibuka homu mambo si yakaanza kujibu yaani noma tupu, mzee mzima nimeumbuka mchana kweupee.. jicho halifai. Au kuna pua ya mtu nini Masela?
Waliomshtukia Mzee wa Kutibua akinyatanyata kwenye korido za tabibu fulani mitaa ya Kinondoni wakamuibukia na kumshauri eti anawie mkojo wa mademu ishu itakata fasta. Eh! Si wana watanikimbia Bongo? Haiwezekani hiyo wakubwa.
Lakini ishu zinasonga ingawa mambo si mambo kwenye waleti za wanangu fulani ambao kupiga mguu siku kama hizi kukatiza mitaa ya Kino kuibukia Dasilamu mjini ni ishu ya kawaida.
Ndio maisha ya bongo hayo, usione jamaa linamwagika jasho ukafikiri ni misosi imekubali. Mambo yametaiti kila kona, nani arudi Itigi aiache Samora Avenyuu Darisalamu. Unacheza... nini!
Ebu ngoja kwanza nkupe ishu! Hawa wababaishaji wanaojifanya wanazipenda timu zao wakiendelea kuendekezwa kwenye uwanja wa Taifa, iko siku watanyonga mtu na mtalia.
Tiefuefu na Polisi fungueni macho, Musiwe wanafiki hivi vitendo vinavyofanywa na mashabiki wa Pan Africa na majirani zao wa Ashanti ni hatari kwa maisha ya binadamu.
Tumekuwa tukishuhudia katika mechi zinazohusisha timu hizo mashabiki wenye jazba wakisogelea mabenchi yao ya ufundi mara kadhaa na kutukana na kutishia makocha na wachezaji.
Baadhi wamekuwa wakikera wachezaji na kuwapotezea umakini wa kusoma na kuangalia kwa kusimama kwenye uzito karibu na mabenchi na kuwatishia.
Lakini cha kusikitisha zaidi tumeshuhudia wengine wakipenya uzio kwa kupitia kwenye geti kubwa kwenda mpaka kwenye benchi kutishia kwa maneno makocha huku wakiwaelekeza kufanya mabadiliko? Nini kazi ya hao Polisi getini?
Vitendo hivyo ambavyo vya kibabaishaji, vinavyofanywa na baadhi ya mashabiki ambao sisiti kusema ni wababaisha ni vya kudhalilisha taaluma kwa makocha husika na kuvuruga wachezaji.
Napata ugumu kuelewa upeo na wanachofikiria viongozi wa klabu hizo ambao kwa mara kadhaa tangu vitendo hivyo vimekuwa vikionekana kwenye uwanja wa Taifa sikupata kusikia au kuona wakitamka chochote. Msafiri vipi bwana! Au ndio kawaida Ki-Ilala Ilala?
Haiwezekani shabiki tena Mzee wa miaka isiyopungua 60 anatoka jukwaani huku akishangilia na wanazi wengine anapenya uzio ulio chini ya Polisi na kwenda kuwafokea makocha kwenye benchi huku ngazi zinazohusika kila mmoja akishuhudia.
Akienda na silaha akamchoma kocha au mchezaji je?Nani atawajibika kwenye hili na ni uzembe wa nani?
Kwanini kila mtu asipewe nafasi na kutekeleza majukumu yake kiufasaha? Hawa wababaishaji wataendekezwa mpaka lini. Kwanza wana mchango gani kwa klabu zaidi ya kujitokeza tu na kuanza kupiga makelele uwanjani, unazi gani huo wa kishamba wakubwa?
Viongozi wa hizi klabu za Ashanti na Pan Africa wanapaswa kuwaelemisha na kuwadhibiti mashabiki wao. Hata Tiefuefu inapaswa kushikilia makali zaidi kwa kuhakikisha kila mtu anakuwa huru kutekeleza majukumu yake na wababaishaji wanaojifanya wana machungu wadhibitiwe na sifa za kijinga ziwaishe.
Haiwezekani watu wenye ‘mamulhaka’ tukalea vikundi vya mashabiki wachache wanaotaka kutuvuruga na kutupotezea uelekeo. Hawana jipya na naamini hata fomesheni pengine hawajui kabisa. Kwanini tunalea uozo kama huu?
Ebwana wanangu eee... naingia mitini kimtindo. Mwanangu Uli, Machupa ...ee..kesho vipi Taifa hapo? Mshkaji wangu Ben, Ngassa...ee inakuwaje Madagasca hapo itakuwaje?
Sasa ni intaneshno mechez kuanzia kesho. Simnajua? Tuache unazi wa kishamba, tuweke mbele uzalendo tushangilie Wanaume wasonge mbele.
Utani sio uadui... achaneni na ushabiki wa mwaka Arobaini na saba mbona mabosi wenu wanakaa meza moja hamuoni hata hao wazungu wanapiga kinywaji pamoja?
Bofya basi kwenye MZEEWAKUTIBUA.BLOGSPOT.COM utaliona laivu zee la Kutibua. Badae kama kawa Kungwasumika Keinyama au Kupekecha Msasani. Redi Aizi kitu gani bwana?ntaibuka we ncheki maeneo maeneo hapo ila tusikerane.
0713374649

Friday, February 1, 2008

Fabio Capello ambania Beckam


KOCHA wa England, Fabio Capello amempiga chini
David Beckam kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya
Switzerland jumatano ijayo. Mashabiki wengi wa nchi hiyo wamekuwa wakimtaka Capello anayepuuza mambo na kushikilia misimamo yake, kumpa nafasi Beckam ili atimize mechi yake ya 100.
"Nimemshauri kwamba yeye ni sehemu ya mikakati yangu na atakapocheza vizuri zaidi Marekani nitamuita,"alisisitiza Capello mwenye miaka 61.

Wednesday, January 30, 2008

Lampard bado aendelea kusugua benchi Chelsea

Hali ya Kiungo wa Chelsea Frank Lampard bado haijatengamaa na huenda akakaa nje wiki mbili na atakosa mechi ya leo ya Ligi Kuu dhidi ya Readings kutokana na majeraha yanayomkabili. Mbali na mchezaji huyo hata Shevshenko na John Terry ni majeruhi.

Bado Arsenal Februari 17 Old Trafford


Man juzi ilipiga Spurs bao 3-1 kwenye michuano ya FA huyu bwana mdogo Ronaldo alipiga mawili na Terves akapiga bao la mwisho. Arsenal alimpiga Newcastle 3-0. Adebayor kapiga mbili jingine jamaa wamejifungua kimchecheto tu.

Sisi ndio yanga bwana..tunatisha


Yanga imefikisha pointi 24 katika msimamo wa Ligi sawa na Prisons inayoshikilia usukani. Lakini vijana hao wa jangwani wamedai kuitoa Prisons kileleni ni kazi ndogo na itaanza ijumaa hii dhidi ya Coast Union.

Dah! Kazi ngumu Man wanakimbia balaa...


Dah! kujikaza kote huko ndio kwanza pointi 39, nafasi ya sita Man U wana 54 yao kileleni tutawakamata kweli....! wasiwasi wangu wasije kumfukuza Benitez wangu tu.
Stephen Gerald-Liverpool.

Sasa sikilizieni makamuzi yangu


Ally Choki ambaye ameitosa Twanga Pepeta International na kuibukia zake TOT Plus ameibuka na kusema kuwa anakuja na madude manne mapya ya kufa mtu na kila mtu atabloo.

Choki ambaye sasa yupo zake mitaa ya Tabora kwenye ziara na bendi yake mpya amemhakikishia Mzee wa Kutibua ambaye ni mpenzi wa dansi kwamba muda si mrefu atavunja ukimya na kila mtu atashika mdomo.

Tuesday, January 29, 2008

Twiga watagoma tena au?


Shilingi mil. 7.5 zimetolewa na Benki ya Barclays kwa ajili ya kuisaidia Twiga Stars kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Cameroon wa utakaochezwa mwezi ujao kuwania tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika.

Wasiwasi wa Mzee wa Kutbua msije mkagoma tena mkifikiri ni za mgawo...!

Oya mshikaji Ulabu gani huo...?

ANGALAU! Lakini dah! Sijui itakuwaje masela, kuna ishu ishu fulani ambazondivyo sivyo kimtindo kwa mwanenu, inabidi tuteme mate chini tu.
Kakikohozi kwa sana na wese linashuka kichizi puani tangu juzi kati hapo,sijui ndio inakuwaje tena mambo kama hayo kwa mtu mzima kama hivi.Au huyu msela hapa kulia anafanya mambo fulani nini nimwachie liuwanja lakujinafasi?
Mambo yamekuwa mazito ikabidi watu wazima wamrudishe bwanamdogo bushi kidogo akaweke mambo sawa. Lakini sio ishu tujifanye hatujui.Basi juzi kati fulani bwana, mida ya jioni nikaibuka zangu mitaa yaUbalozi (jirani na hiyo klabu wanaita Lidaz) kule Kinondoni kwa nyumanyuma hivi sehemu fulani wanaita Octa Contena wanakoutwika wajanja.

Nilikuwa na mtu kama tatu zenye nyadhifa zao kwenye ofisi nzito nzito hukotawni ambao hata kuvusha wiki wakiutwika ‘twenti fo Awaz’ na kuegesha juuya meza kwao siyo ajabu.
Wakati watu wazima tunazidi kujinafasi na mamonde yaliyotanda zake mezani,kumbe bwana meza ya pili kuna masela fulani hivi kama wawili (nimetonywani Mapaparazi wenye maujiko ya kufa mtu Bongo hapa) mmoja kautwika zakemadude fulani hivi yanakaa kwenye maboksi(wanaita Penasoli sijui…kitu kamahicho) nafikiri kuanzia moningi jamaa anayagonga tu kwa mujibu wa wadau.
Kuna vagi kimtindo jamaa anakuja juu, hata macho hayataki tena kuona, basimwana mida hiyo masela huku pembeni burudaani… jamaa kazidiwa kanyanyukakwa msaada anaoujua mwenyewe kaibuka zake toileti.
Ni mida fulani ya saa mbili na ushee, masela zake wakangoja wee bila bilawakadhani labda jamaa kamwagiwa tindikali na Mafisadi au Jamaa fulaniwaliolamba mabilioni ya Biotii wamemzamisha toileti ili azibe mdomo,ikabidi wamuibukie.
Kumbe bwana msela maji yamezidi unga alipotoka zake kupunguza Toi,kasahau alipokuwa ameegesha kapapasa papasa geti la uani katokea Baa yajirani nako bado chaneli ikawa haikamati akaamua kutoka nje akaegeshakwenye lami ya Alhassan Mwinyi.
Duh! Blaza vipi tena?Mungu saidia Dada nanihii katafuta kichizi kila mahali kakosa,alipobahatisha Baa ya pili akaambiwa kuna msela alipita na ukuta hapamcheki labda rodini. Duh jamaa akanaswa bwana kaegesha rodinialiporejeshwa kwa masela wake anacheka mbavu hana…, nini kisa eti alijuayuko kwenye taxi anaenda Mwenge.
Duh! Blaza inakuaje ukinywa za uswahili?Uchune kidogo nikuambia ishu nyingine. Kiligi chetu cha Bongo ujuekinaanza leo kimtindo, wenye kupenda lahaa… tunaibuka zetu badayegraundini tukaangalie boli la wanetu siunajua tena tulikuwa tumelimisimida?
Lakini wana mmepiga matizi mwezi na ushee hatutaki kuona madudu na ushenziushenzi usiona na maana kama ilivyokuwa kwenye mzunguko ulijikata mwakajana ambao watu wazima Lunyasi na Jangwani walikiona cha moto kwa haowaliokuwa wakidhani ni mabwana wadogo.
Ubabe siyo ishu badilikeni wanangu, pigeni boli la akili kama tunalochekikwenye kideo huku Ghana, mangumi na kukanyagana kanyagana sio dili. Ndiomaana mnazidi kubanana Bongo tu na utajiri wa kutembelea Baluni na vyumbaviwili uswahilini.
Badilikeni mchezee mpira si miili ya watu, tumieni akili na vipaji vyakuzaliwa wazee sisi tunatoa mkwanja wetu hatuji kuuza sura tunakata kuonagemu tufurahi na magoli yafungwe si papara za ajabu zisizo na akili.Tulizeni akili msikilize mnachoambia na Maticha mtufanyie mambo, sisimkiendekeza ishu za ovyoovyo kama lasti raundi sisi tutakupigeni chini tukama vipi.
Tunakaa Baa tunapiga zetu ulabu na kuangalia kina Drogba, Eto’o na Kanuti. Haturembi simnajua zetu!Msiwe mizigo washikaji fungueni akili kuna ulaji kinoma Taifa Stars,muonyesheni mambo Maximo mle shavu na soka yetu ikue.
Ndio tunachotaka,ishu za ujiko ni baadae.
Ndio wakati wa kutuliza akili, kucheza na kuachana na mambo ya ajabu.Halafu kitu kipo laivu kwenye kideo cha Gitivii mjue! Ndio nafasi zenyeweza kujiuza nje hizo, onyesheni kujiamini mbona Kenya na Uganda wanaibukanje kibao na kufanya mambo kwani wenyewe wana miguu ya plastiki.
Acheni papara na anasa zisizo na msingi hiyo ni kazi wakubwa, tumieniutashi kuweni na ari ya mabadiliko tunakokwenda ni kugumu kichizi na umriunazidi kuyeyuka.Imefika enzi za wachezaji kubadilika na kuishi kama binadamu wa karnempya, msiridhike na maujiko ya uwanja wa Taifa mabega yakazidi vichwamkasahau kwamba kuna leo na kesho na maisha yako kama mchezaji yako miguu.
Kwamba mchezaji unaweza kuwa na mafanikio wakati ukiwa kwenye fomu keshona keshokutwa mambo yanaweza kubadilika. Na hivi wakazidi kuingia makochaWazungu patakuwa hapatoshi mkiendekeza uvivu na usupastaa wa kununuliwaKilimanjaro Uswahili mtaona Bongo chungu.Mtajichuja.
Na kwanini ifikie hatua hiyo? Wakati mna kila kitukinachostahili kwa nyie kibadilika na kufikia kwenye hatua inayokubalika.Oya washikaji pigeni kazi, embu jiskieni haya kidogo basi tupige na sisihatua kimataifa, kwanini mashabiki wenu wawe wawe wapweke kila sikukomaeni mtuinue Wabongo wenzenu wana.
Nasi tucheki wani dei. Mwanangu Songoro mitaa ya Chaga Baiti, Wili kwa Mapecos hapo na Wazee waNewvision, Sayansi kwenye kitimoto sana… tu! Leo Mtaumia, Mcameruni wenuatachomoka kwa Zambia iliyompiga Sudan tatu kwa mtungi?

Hawa ndio cameroon bwana!


Lwakatare naye ndani ya nyumba


Mbunge wa viti maalum, mchungaji Getrude Lwakatare akila kiapo jana Bungeni mjini Dodoma. Ameziba nafasi ya Salome Mbatia aliyefariki hivikaribuni kwa ajali ya gari.

Hawa ni Simba Wako Coco Bichi bwana wanajifua!


Nyagawa alivyozamisha kitu langoni


Kiungo mshambuliaji wa Simba Nico Nyagawa alipomtoka, kipa wa Coast Union Ismail Suma na kupiga kitu nyavuni na kuandika bao la kwanza kwa wekundu wa Msimbazi hapo Taifa. Simba ilishinda 2-1.

Twiga Stars wana uelewa mdogo-TFF


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema uelewa mdogo wa wachezaji ndio uliosababisha kutishia kugomea kambi ya timu hiyo iliyopo kwenye hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa TFF Frederick Mwakalebela alisema wachezaji hao kwa upeo wao walidhani shilingi milioni 2 zilizotolewa na mke wa Rais Mama Salma Kikwete ni motisha yao kwa kuwafunga Eritrea.
"Uelewa wao mdogo ndio walitaka kugoma, walidhani zile hela zilizotolewa na Mama Kikwete ni zawadi yao walipoifunga Eritrea."alisema Mwakalebela ambaye ana kitambi.
"Zile fedha zilipoletwa nilimwambia meneja wao awalipe posho yao yote pamoja na walimu zilibaki laki moja nikamwambia ajaze yote mafuta basi la wachezaji linalowapeleka na kuwarudisha mazoezini.
"Mama Salma Kikwete alipotoa zile hela alisema ni za kuisaidia timu katika maandalizi yake dhidi ya Eritrea sasa wao kwa upeo wao sijui walivyoelewa wakahamasishana wakataka wapewe zile hela zote wagawane kama motisha wao wa Eritrea."

Aisha Madinda:Wameniambia niokoke nipone


“Nimepokea simu kwa mamia na meseji nyingi sana, ila kuna wasamaria wamekuwa wakinishauri mara kwa mara kwamba niokoke na kumrejea Mungu kutokana na hali niliyonayo.
“Wanasema kwamba endapo nikifanya kitu kama hicho naweza kupona haraka na kurejea kwenye hali yangu ya kawaida mapema kila mtu amekuwa akitoa maoni yake na nimekuwa nikiwaskiliza.
“Lakini bado sijaamua nini cha kufanya bado nataka kuzingatia matibabu ambayo nitakuwa napewa na madaktari wa Muhimbili kwanza halafu nione nini kitakachofuata lakini nina imani kwamba ipo siku hali yangu itakuwa vizuri,"Aisha alimwambia Mzee wa Kutibua jana jijini Dar es Salaam.

Mwanamama huyo mwenye watoto wawili wanaosoma sekondari amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya moyo kujaa maji na miguu yake sasa imevimba kiasi kwamba anashinda hata kuvaa viatu wala hajaenda kwenye maonyesho kama miezi mitatu sasa imepita. Baaadhi ya wanyetishaji wasio na dogo wamekuwa wakiihusisha hali yake na imani za kishirikina.

Hatari ya Athuman Iddi! Aisee..!


Athuman Iddi wa Yanga alipogongana na mchezaji wa Ashanti na kuumia vibaya kwenye mechi ya kwanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara. Hakukuwa na watu wa huduma ya kwanza kwenye uwanja wa Taifa siku hiyo na ililazimika mchezaji wa Ashanti kukimbizwa hospitali kwa gari binafsi ya shabiki mmoja. TFF why....kwaniniiiiiiii?

Shughuli iliyomleta ulimboka stars


"Hii najipinda halafu naizungusha, nachomoka hivi, mi ndio ulimboka bwana ukisikia mwingine ni photocopy."
Jamaa anasemaje unajua: Nimefurahi sana, huu ndio wakati wangu wa kuonyesha mambo adimu .

Nataka Stars hii iwe juu sana




''Nimwachanganya kikosi changu kina wazoefu wachache na vijana wengi lakini nimefanya hivi ili hawa wenye uzoefu waweze kuwaongoza hawa vijana, lakini wanatakiwa kuonyesha uwezo wao uwanjani ili waweze kudumu kwenye kikosi cha Stars" alisema Maximo alivyotaja kikosi chake kipya jana kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi Februari 6.
Makipa -Ally Mustapha Simba , Farouk Ramadhan Shaaban Dihile JKT Ruvu.
Mabeki- Amir Maftah Nadil Haroub 'Cannovaro' (Yanga ) Said Swed (Simba) Meshack Abel, Salum Swed (Mtibwa) Salvatory Mtebe (Atraco) Erasto Nyoni (Vital o) Dennis Mukebezi (Coastal Union) na Stephano Mwasika (Prisons).
Viungo-Abdi Kassim, Athumani Idd, Castory Mumbala (Yanga) Ulimboka Mwakingwe Haruna Moshi na Henry Joseph (Simba) Shaaban Ndity na Kigi Makasi (Mtibwa Sugar) na Nizar Khalifan (Kuwait).
Washambuliji -Danny Mrwanda (Kuwait) Jerry Tegete na Vicent Barnabas, Yanga Athuman Machupa (Simba) na Uhuru Suleiman Coastal Union.