Friday, November 2, 2007

Hii ya Nsajigwa na Ivo ni kafara

HEE..! Washikaji ndio Novemba hilo ndani ya nyumba kama masihara vile, wazee wazima ndio tunazidi kwenda eji tu kiutani utani mara unakuwa zilipendwa.

Ndio muda wa mahesabu unakaribia wanangu na mambo ya minuso minuso ya klithmasi araundi ze kona kazi kwenu sasa, ila kazi ipo unaweza kujikuta ukijibinafsisha hivi hivi.

Mambo yako kwenye mstari kiaina kwa Mzee wa Kutibua na angali akidunda uraiani kwa jeuri ingawa jua la Bongo linazingua upara wake. Si unajua aliamua kulikwaruza baada ya vinyweleo vyeupe kuanza kumnyemelea?

Ngoja nikumegeeni kwanza hii! Siku kama nne hivi zilizopita Mzee mzima niliibuka kwenye Kabaa fulani hivi mitaa ya Keinyama hapo, kwa mualiko wa mzito wa mdau fulani wa muziki wa bongo.

Siunajua tena mwanangu sehemu kama hizo, kilaji na mambo fulani fulani si ya kuuliza? Kwenye meza wapo washikadau kama wanne hivi.(ukijiskia waite kwa majina yao ya serikali.. Shekigenda, Babuu, Tesha na huyu wa mwisho nani huyu … Lucas).

Usimhesabie huyo Byarugaba ambaye alianza kutwanga nanihii..Kesto tangu mida ya lanchi alipoenda kwenye Eitimu akakuta Mpunga wa mwezi tayari umeshajaa. Yeye tayari kashazimia kitaambo, kaegemea kiti. Kinachotoka mdomoni ni kauli moja tu “…mmhh!”.

Walioko kwenye meza ya Mzee wa Kutibua ni wazito na jamaa fulani fulani huku pembeni shingo ni nyingi zinahaha kuangalia mchakato unavyokwenda, pengine ni kutokana na mijusi mizito waliyotinga washikadau ambayo kwa kawaida ya kiwanja tulichopo inahesabika au wakati mwingine haipo kabisa.

Ghafla huku nyuma kaibuka jamaa (rapa wa bendi moja hapo kinondoni) wa bendi maarufu ya Bongo kaanza kutoa salamu akiwa mita kama mia hivi “Pedeshee Shekii…, Pedeshee Shekii…” Tesha akasemaa ohooo… “kimechafuka, mtu wa mizinga huyo kashavamia, hakawii kugeuza steji hapa”

Jamaa kama vile kazilalia sana jana anavyoonekana halafu bigi chachaa mifukoni, kabla ya kupiga mzinga dada nanihii ambaye amekulia ng’ambo ya bahari (Mkunazini) kashafika karibu akamhudumia, jamaa si akaanza kuzichapa kwa hasira kama anakomoa!

Kafyonza hizo wanazoita nondo kama nane ivi ndani ya dakika chache, hajui kama kuna mnene aliyemtengea fifte ya kumkomesha, ameanza ya tisa tu hoi ngoma ikaanza kuzomea sakafu.

Ayaah…! Aibu.. watu wote mikono mdomoni wanashangaa, mambo si mambo mtu mzima kashaharibu faragha hakieleweki tena wala hata macho hataki kufungua. Kwa umbaalii anasema eeehh.. eehh! Mwanangu aibuu… watu wamebeba kama nanihii.

Lakini..! Ebu ngoja tuchenji chaneli kwanza, siku siyo nyingi sana Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa wamefungiwa na klabu hiyo miezi sita kutokana na mambo kibaaoo moja wapo likiwa ni madai ya hujuma na utovu wa nidhamu.

Wachezaji hao wanadaiwa kuhujumu timu hiyo ikafungwa na Simba 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Bara wiki sio nyingi zilizopita huko Morogoro na baadae kutoroka kambini bila taarifa kitendo kilichotafsiriwa kama utoro kazini na utovu wa nidhamu.

Wadau wa soka ambao hawafungamani na upande wowote walionyesha kushangazwa na kitendo cha kundi la mashabiki wa Yanga kumvamia na kumpiga vibaya Mapunda baada ya mechi hiyo kwa kile walichodai kuwa aliwafungisha, huku wachezaji kadhaa nao wakiambulia matusi na wengine wakitembea si mita nyingi na Polisi wakutuliza ghasia.

Lakini cha ajabu na ambacho kinashangaza wengi Ivo angeweza hata kufa kwa ajili ya makosa ya kibinadamu ya sekundu moja tu akiwa langoni. Kwanza hakuna kiongozi yoyote wa Yanga aliyeonyesha ubinadamu kwa kuibuka na kumnusuru Ivo alivyokuwa akipambana na mashabiki je? Kama si Polisi waliofanya jitihada za makusudi nini kingetokea kwa kipa huyo wa timu ya Taifa.

Achana na hilo, viongozi hao hao ambao ndio wanaowajibika na usalama wa mchezaji mbali na kwamba hata kambini hakuna aliyefika kumjulia hali kibinadamu baada ya mchezo huo, hakuna pia ambae aliyekuwa akijali hali ya vitisho kwenye simu na mitaani alivyokuwa akipata mchezaji.

Sasa katika mazingira kama hayo, unategemea mchezaji aendelee tu kuendelea kuishi kambini na kuitumikia timu katika mazingira gani wakati hata kocha mwenyewe, ameshanukuliwa na vyombo vya habari akidai kwamba ni kosa la kipa limewanyima ushindi?

Hali hiyo ndio iliyowakumba na wachezaji wengine kama Nsajigwa na Amir Maftah ambao waliamua kuingia mitini. Ingawa Maftah hajafungiwa kwa madai kuwa bado hajaitwa kujieleza.

Lakini kinachoonekana ni kwamba viongozi wa Yanga wamewahukumu wachezaji hao kwa kutumia propaganda za kiuongozi zaidi na hawana sababu za msingi za kisomi ambazo ukiwakurupusha hata sasa wanaweza kukuambia ukaridhia.

Mazingira hayo ndio yanafanya wadau wa soka na wenye upeo mkubwa kwenye masuala ya kiuongozi waamini kwamba wachezaji hao wametolewa kafara ili kulinda maslahi ya viongozi mbele ya wanachama, ambao wiki chache zilizopita walikuwa wanavurugana wenyewe kwa wenyewe.

Hakuna mwanamichezo asiyeelewa kwamba mpira ni mchezo wa makosa na huwezi kuwa juu siku zote ndio maana kukawa na usiku na mchana, hakuwezi kuwa mchana tu siku zote. Mbona Lehman wa Arsenal amefungwa mabao ya kizembe mechi kama nne mfululizo hatujaskia amesimamishwa miezi au hata kutozwa faini.

Paul Robison wa Totenham Hotspurs ambaye kila mechi anafungwa bao la kizembe mbona hatujaskia kaadhibiwa? Tena kasajiliwa kwa mabilioni sembuse Ivo wa Tukuyu ambaye hata glovu za mazoezi ananunua kwa machinga Kariakoo?

Achana na hao Richard Micah beki tegemeo wa Manchester City (kama ilivyo Nsajigwa kwa Yanga) ambaye yeye pamoja na wenzake wamefanywa uchochoro wakapigwa 6-0 na Chelsea stanfodi briji, angekuwa Yanga ingekuwaje?

Sipingi kwamba uongozi unaweza kumpa mchezaji adhabu kama muajiri na muajiriwa lakini si hii ya miezi sita ya Ivo na Nsajigwa iliyotolewa na uongozi wa Madega, ni kuua vipaji vya wachezaji na ni ubabe pia, kufungwa na Simba sio mwisho wa Dunia. Msiendekeze kelele za mashabiki wachache ambao wana maslahi yao.

Achana na umuhimu wao Taifa Stars, inawezekana kuna makosa yamebainika kwa utashi wa viongozi lakini kwanini wasingepigwa faini au kukatwa mshahara kwa miezi hata miwili kama inavyofanywa kwenye nchi zilizoendelea kuliko kutoa adhabu kama tunazoshuhudia ambazo siogopi kusema ni za kizamani na za kienyeji.

Halafu isitoshe viongozi hao hao wanakwenda Tiefuefu kuomba kipa wao aliyefungiwa mechi sita, Benjamin Haule afunguliwe ili wamtumie kwani ni hatari kubakiwa na kipa mmoja (Jackson Chove) ambae baadhi wanadiriki kumuita “namba tatu”. Kwani wakati mnamfungia Ivo hamkujua hilo na huyo?

Imefika wakati viongozi wa klabu za Tanzania kubadilika kifikra na kufanya mambo kisomi badala ya kutumia propaganda. Siwafundishi wajomba hizo ni salamu zangu kwenu.

No comments: