Friday, December 7, 2007

Jiandaeni kupambana na wanaume akyanani!

MUNGU mkubwa ! habari ndio hiyo kwamba pasipo yeye hakuna kitokacho wala Mzee wa Kutibua asingeweza kuvuma chini ya hili Jua la Bongo ambalo ni 'ova balaa'.
Ndiyo ukweli ulivyo kwamba mambo yamechengi na kimechafuka ndani ya ardhi ya wabongo ndio maana washirika fulani wa Mzee wa Kutibua wameanza kurejea maisha ya bushi.
Lakini mambo ya Mzee wa Kutibua yapo kwenye mpango sahihi na maisha yanasonga kwenye mpango sahihi.
Wala usione soo ndio ishu zenyewe kwamba kuna wakati wa kutembea na kukimbia hata kulia na kucheka ndio maana si ajabu kuona wenye suti zao huko katikati ya Jiji wakigombea Magobore ya kuelekea Shamba.
Au wajanja ambao mida kama hii wamejimwaga kwenye viwanja vyao vya kutumia wakitamba kwamba Noeli ndio imepamba moto huku wengine wakisugua lami huko Samora kuhakikisha kwamba mambo yanakuwa mambo kabla hakijaharibika .
Lakini ikiachwa hiyo ishu, mlichokuwa mkikisubiri kwa hamu ndio hicho sasa kazi kwenu. Ngoma uwanjani mpaka kieleweke Mwekundu wa Msimbazi kivyake na Wanjano Jangwani kinyake.

Simba imepangwa kukipiga kwenye klabu bingwa na Awassa ya Ethiopia na Yanga wanatifuatana na mwakilishi wa Chad au Al Akhdar ya Libya kwenye raundi ya pili ya kombe la Shirikisho kwa vile mwakani iliishia kwenye raundi ya tatu ya Mabingwa na Shirikisho.

Kipute hicho nguo kuchanika, kinaanza mapeema Februari mwakani huku timu nyingi maarufu zikiwa zimefuzu kuziwakilisha nchi zao safari hii hiyo ikimaanisha kuwa patakuwa hapatoshi kama wanavyopenda kutia msisitizo vijana wa tawni.

Simba na Yanga na zenyewe tayari zimeanza maandalizi ya hapa na pale lakini bado hayajafikia kiwango cha kutupa matumaini ya kuona mabadiliko katika michuano ya kimataifa mwaka huu na wala zisitegemee kwamba mwezi Februani ni mbali.

Simba ambayo imekuwa na rekodi ya kuridhisha kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, yenyewe hata haijaingia kambini na tumekuwa tukishuhudia ikifanya mazoezi yake kwenye uwanja wa Tanganyika Parkers jijini Dar es Salaam na kucheza mechi za kirafiki.

Hatukatai kwamba mechi hizo nazo ni muhimu haswa kwa kujenga timu lakini zisiwadanganye, viongozi na hata makocha wanapaswa kutambua kwamba kambi ni muhimu zaidi si tu kwa ajili ya kuwapa maarifa zaidi wachezaji bali kutambua kiundani hali halisi ya kila mchezaji na kuijenga timu kiufundi zaidi.

Na huwezi ukajiridhisha kwamba una timu nzuri kwa kuangalia majina uliyosajili, ingiza timu kambini uisuke. Hao wachezaji wapya walioongezwa wanapaswa kuwekwa pamoja wenzao, hata Arsenal, Chelsea, Manchester United, Liverpool zenye mastaa kibao zinaheshimu sana suala la kambi.

Huwezi kuweka kambi ya wiki mbili au tatu na kutegemea kufanya vizuri na kuwa na kikosi makini kama mshindani wako au klabu zingine zinazoshiriki michuano hiyo ambazo sasa zipo kambini baadhi ndani ya nchi zao na nyingine nje.

Tuepukane na tabia ya kulipua mambo au kusingizia njaa ya pesa, klabu kubwa kama Simba ikiwa na mazingira mazuri ya kiutendaji na watu makini wanaojali haiwezi kukosa wadhamini watakaomwaga mapesa yatakayoiwezesha kujiendesha kisasa zaidi.

Vurugu za kila leo baina ya viongozi ambazo husababisha kutoelewana ndizo zimekuwa zikiwakatisha tamaa wenye pesa zao kuja kuwekeza kwa vile wanahisi zitatumbuliwa na wajanja wachache au ndio zinaweza zikakuza mgogoro mwingine ambao hauna manufaa kwao.

Simba au Yanga ni klabu kubwa nchini ambazo matajiri wenye biashara zao wanataka kujiingiza ili kuhakikisha kwamba mambo yao yanakwenda sawa lakini mazingira yanakuwa kikwazo na sijui kwanini viongozi waliowekwa madarakani kwa dhamana ya wanachama hawakai wakalitambua hilo.

Kwa jina tu la Simba lilivyo ndani ya nchi haiwezekani ikawa haina hata basi la wachezaji, wachezaji wanapanda daladala wanakwenda mazoezini halafu baada watoke waanza kugombania daladala za kuning’inia karne hii? Na Mishahara yao walipeni kwa wakati pia waishi maisha bora..! alaa.

Tujaribu kubadilika na kujiendesha kisasa zaidi tufike waliko wenzetu, huwezi kuwa kwenye kipindi kigumu kama hiki cha kuelekea kwanza kwenye michuano ya kombe la Kagame Januari halafu Februari klabu Bingwa Afrika unampigisha mchezaji zoezi Kawe halafu jioni unamuachia akarande uswahili. Mnataka kutuitia aibu au?

Mnaweza kusema ni jukumu la kila mchezaji kujichunga lakini mchezaji unayemfanyisha zoezi una uhakika gani kwamba baada ya kuachana na wewe(Kocha, Kiongozi au Daktari) anakwenda kupumzika? Kama anautwika na mpaka usiku wa manane je?

Hatusemi kana kwamba hatuna mifano halisia, tunaona kila siku huku uswahili ! Ndio timu ambayo tunategemea itwae ubingwa wa Afrika? Cheameni Dalali upo hapo? Mnachofanya sasa ni kama kucheza kwenye mdomo wa Mamba mwenye njaa, nini unachotegemea?

Hata Yanga ambayo tayari ipo kambini jijini Mwanza chini ya Kocha wa kizungu, Condic Dusan inapaswa kuwa makini zaidi na kuhakikisha kwamba inawatengenezea wachezaji mazingira mazuri ambayo yatawafanya waelewe kirahisi wanayofungwa na mzungu.

Kuingiza timu kambini haitoshi watu watekelezewe matakwa yao muhimu zaidi ikiwa ni maslahi yao, huyo kocha hawezi kufanikiwa hata kama ana mbinu zinazozidi za Alex Ferguson wa Machester au Arsenal Wenger wa Arsenal endapo atakuwa anafundisha watu wenye matatizo na kulazimika kuuchuna kutokana na nidhamu ya woga.

Makocha hao wanaodaiwa kulipwa mamilioni ya shilingi za kitanzania watafanikiwa endapo kutakuwa na mazingira mazuri ya kazi kubwa ikiwa ni hilo la wachezaji kutengenezewa maisha bora.

Yanga na Simba zinatakiwa kuacha masihara hii ni soka wala siyo biashara ya nazi? Halafu kila mmoja anapaswa kutafuta mechi nzuri za kujipima nguvu ili uonekane udhaifu uko wapi! Huu si wakati wa mazoezi ya mbembwe au mechi za kufurahisha mashabiki. Mtaaibika.

Hii ndio nafasi pekee ya kuthibitisha ukongwe wenu ndani ya Tanzania hata Afrika nzima iwatambue na viongozi wajaribu kuwajenga mashabiki wao wawe na nidhamu na uzalendo.

Mambo ya Simba ikicheza Yanga inazomea au Yanga inacheza Simba inazomea, kuhujumu na kushangilia wageni ni mambo yamepitwa na wakati tupeane changamoto ya ukweli, tupige hatua tutoke kwenye enzi za ushabiki wa kishamba tulionao.

Tupingane, tugombee wachezaji, tuchekane nje ya eneo la uwanja lakini inapofika ndani ya uwanja tubadilike tuige tabia za wenzetu kwenye klabu za Afrika ya Kati. Turingiane mitaani kwa rekodi si kuhujumiana hii ni karne mpya.

Ebwana...eeh. Ni hayo tu! 0714878817
mzeewakutibua.blogspot.com

No comments: